VITABU

UNYOOFU UNAAMINI NINI?
 

Uelewa mzima wa Unyofu. Kwanza kabisa dini ya Unyofu haina kitabu. Unyofu hauna kitabu. Sisi Wanyofu tunawajibika kuuamini ukweli na sio kuamini kitabu fulani. Hatuwajibiki kwa kitabu chochote bali tunawajibika kwa ukweli wowote. Ukweli kama ulivyofunuliwa kwetu kupitia ufahamu na kuhakikishwa kuwa ni sahihi kupitia sayansi asili, sayansi Jamii, sayansi ya kiroho na sayansi akili. Ukweli daima unaongezeka na uelewa unabadilika na ikiwa tutawajibika kwa kitabu fulani tutaachwa nyuma, kifungoni mwa kitabu hicho. Kwa sababu kitabu ni matokeo ya maarifa ya kizazi husika, ukweli ukiongezeka kuhusu asili ya ulimwengu, Mungu na binadamu, maarifa ndani ya kitabu hicho yatakuwa yamepitwa na wakati.
 Kwa sababu twawajibika kwa ukweli, maarifa yakiongezeka na kuthibitishwa kuwa sahihi, twawajibika kuangusha kimya kimya na bila ubishi wowote Imani fulani tuliokuwa nayo hapo kabla kwa sababu Imani hiyo haipatani na ukweli uliohakikishwa, na kwa sababu lengo letu sio itikadi bali lengo letu ni ukweli
Sisi Wanyofu tunaamini kwamba Uungu ni mmoja, hakuna asili mbili zenye uungu na hivyo hakuna ushindani wowote miongoni mwa uungu. Sisi hatuna Mungu wetu na Mungu wa wale kana kwamba kuna Mungu zaidi ya mmoja.  

(Bofya hapa kusoma kuhusu kiumbe shetani.)

VITABU, UKWELI & DINI
Miongoni mwa makosa makubwa waliyowahi kufanya wanadini wa kale ni kuufunga ukweli. Waliufunga ukweli ndani ya waasisi wao. Maandiko ya waasisi yakawa ndio yakawa mwanzo na mwisho wa mambo yote. Uelewa waliokuwa nao waasisi ukawa ndio kipimio cha ukweli kuhusiana na Mungu, mwanadamu na ulimwengu. Hawakuruhusu uelewa kuendelea kuongezeka. Kimsingi sayansi pamoja na dini zilipatikana kama matokeo ya ya utafiti wa mwanadamu wa kale kuelekea Mungu, ulimwengu, mwanadamu na maisha. Kwa hiyo dini na sayansi ni elimu kama elimu nyingine zote na kwa hiyo zina sifa ya kukua na kuongezeka katika maarifa yake na badiliko la uelewa. Sayansi imekuwa ikikubali kubadilika na kupokea maarifa na ur mpya, lakini dini imekuwa na misimamo ya kihafidhina na isiyokubali kukosolewa. Wakati fulani ktk historia walijikokeza wanasayansi wawili yaani Nikolaus Kopenicus na mfuasi wake Galileo Galei, watu hawa walisema kwamba wamegundua kwamba kumbe jua ndio lipo katikati ya mfumo wetu huu na sayari zote ikiwamo dunia zinalizunguka jua. Matokeo yake yalikuwa kutengwa kanisani na kuhukumiwa uzushi. Baraza hili la kuhukumia wazushi lilimhoji ni kwa nini Galileo aende kinyume na maandiko yanayosema jua linazunguka mbingu nzima na lenye uhodari katika mbio zake kama shujaa. Na pia kwamba Yoshua alisimamisha jua na mwezi na sio dunia na mwezi na maandiko yanasema kwamba kweli jua likasimama. Katika majibu yake Galileo aliwajibu kwamba ni kweli Biblia imesema hivyo lakini macho yake yameona kitu tofauti.
Ni kosa kubwa lenye kuzuia makuzi ya ufahamu kufanya uelewa wa kizazi fulani kuwa kipimio cha ukweli. Hivyo dini imechangia pia kuchelewesha maendeleo kwa sababu ya kudumaza fikra za waumini wao. Sisi Wanyofu tunaamini kwamba maendeleo ya binadamu katika nyanja zake zote ndio yatakayomletea Ukombozi wa kweli dhidi ya matatizo yote yanayomkabili hivyo kuufungia uelewa mahali fulani ni kuuchelewesha Ukombozi wa mwanadamu.

Ukweli ni suala endelevu na hivyo halipaswi kufungiwa ndani ya mtu mmoja, kizazi kimoja au taifa moja. Kwa sababu kila kizazi kilichokuja duniani kilikuja na ukweli mpya ambao haukuwa ukijulikana hapo kabla. Tunachoweza kusema ni kwamba kila kizazi kimechangia katika maendeleo ya ukuaji wa ukweli. Hakuna kizazi ambacho kilikuwa kikijua mambo yote bali ukweli ni matokeo ya mchango wa vizazi vyote kikiwemo hiki tulichomo na vizazi vitakavyokuja kwa hio ukweli ni suala endelevu.

Kwa sababu hiyo sisi Wanyofu kama dini hatuna maandiko fulani matakatifu kipimio cha ukweli. Kila maandiko yana expiry date, kwa sababu kile kilicho ukweli leo kesho kitasahihishwa na kuhitaji maboresho. Kila maandiko yana uelewa sehemu kutokana na uelewa wa wakati husika na kadiri muda utakavyozidi kusonga ndivyo uelewa utakavyozidi kubadilika na maandiko hayo kuzidi kutokufaa kuwa kiongozi wa watu tena. Na kwa sababu hiyo hayatafaa kuwa kipimio cha ukweli cha vizazi vyote.
Sisi Wanyofu hatuwezi kuangukia katika kosa hilo la kuufunga ukweli na kuunyima nafasi ya kukua. Sisi Wanyofu si waumini wa maandiko bali ni waumini wa ukweli kwa sababu ukweli ndio lengo letu.

 

No comments:

Post a Comment